Tuesday, November 26, 2013

MAUAJI NA MASHAMBULIO DHIDI YA WAPENZI NA UNYANYASAJI WA KINGONO VINATISHIA AMANI NCHINI

MFANYABIASHARA maarufu mjini Tabora, Hakimu Hamdun, mkazi wa Kata ya Kanyenye anashikiliwa Polisi akituhumiwa kujaribu kujiua kwa kujipiga risasi kutokana na wivu wa mapenzi.
Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Kamishna Msaidizi, Peter Ouma, alisema kuwa Hamdun alijaribu kujiua kwa risasi wiki iliyopita saa kumi na mbili jioni nyumbani kwake eneo la Kanyenye mjini hapa. 
Alisema kuwa Hamdun ambaye kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Mkoa Kitete kwa matibabu, alijipiga risasi baada ya mkewe aliyempa talaka mbili, kumtaka afuate utaratibu wa ndoa ili warudiane.
Inadaiwa Hamdun alimpa talaka mbili mkewe huyo, Joha binti Sudi, lakini baadaye alibadilisha mawazo na kumtaka warudiane huku akimtishia kumuua kama asipokubali.
Kwa mujibu wa madai ya Kamanda Ouma, wanandoa hao waliotalikiana walikuwa wanaishi nyumba tofauti na Hamdun aliamua kumfuata mkewe alipokuwa akiishi akiwa na gari lake na kumtaka warudiane. Hata hivyo, alidai mkewe huyo alikataa kurudiana kienyeji na kumtaka Hamdun kama kweli anampenda, afuate utaratibu wa Dini ya Kiislamu ndipo watimize azma yao hiyo ya kurudiana.
Utaratibu Utaratibu huo kwa mujibu wa dini ya Kiislamu, talaka moja na mbili zinaitwa talaka rejea, ambapo mume aliyotoa talaka hizo, anapaswa kumpa chumba mkewe pale pale nyumbani wanakoishi na chakula kwa miezi mitatu (eda). Ndani ya hiyo miezi mitatu, ikiwa watataka kurudiana, mume huyo ataruhusiwa kwenda katika chumba cha mkewe na kumtaja kwa jina lake na kutamka nimeamua kukurejea. Kwa taratibu za imani ya Kiislamu, mke hatakiwi kukataa na hilo linapofanyika halihitaji shahidi wala shehe. Ikiwa mke atapewa talaka tatu, atakaa eda akila na kuhudumiwa kila kitu mpaka miezi mitatu iishe, ambapo mwanamke atasafiri kurudi kwao. Kama mume atataka kumrejea, mke huyo atapaswa kuolewa kwanza, aachike ndipo utaratibu wa kufunga naye ndoa uanze. 
Badala ya kufuata utaratibu, inadaiwa Hamdun alienda kwenye gari lake na kuchukua bunduki aina ya Shot gun na kwenda nyumbani kwake ambapo alifunga milango, akajipiga risasi katika ubavu wa kushoto. 
Kwa mujibu wa Kamada Ouma, mtuhumiwa huyo hali yake inaendelea vizuri lakini amepoteza sifa ya kumiliki bunduki na hivyo hatapewa tena. 
Aidha, Hamdun atakapomaliza matibabu atafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yake ikiwemo ya kutishia kuua na jaribio la kutaka kujiua.

HabariLeo

AMUUA MKEWE KWA KUMCHOMA KISU MBARALI, MBEYA

Gervas Kadaga

MWANAMKE mmoja mkazi wa kijiji cha Mahango kata ya Madibila wilayani Mbarali mkoani Mbeya aliyefahamika ka jina la Jitihada Mamga(20) ameuawa kwa kuchomwa kisu na mumewe aliyefahamika kwa jina Gervas Kadaga(25) ambaye pia ni mkazi wa kijijini hapo. 
Tukio hilo limetokea Novemba 21 majira ya saa 1:00 jioni baada ya kutokea ugomvi baina ya wapenzi hao ambapo marehemu alikutwa na majeraha tisa ya kisu katika sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Bw. Diwani Athumani alisema kuwa marehemu alifia nyumbani kwake ambapo mtuhumiwa ambaye amelazwa katika hospitali ya Rufaa Mbeya naye amejeruhiwa kwa kuchomwa na kisu tumboni.

Hata hivyo Kamanda Athumani alisema kuwa hadi sasa hakijafahamika chanzo halisi cha ugomvi huo ambapo Jeshi la Polisi linaendelea kufanya uchunguzi wa tukio hilo huku mtuhumiwa akiwa amewekwa chini ya ulinzi wa polisi katika hospitali ya rufaa ya Mbeya alikolazwa.
Akizungumza katika hospitali ya rufaa alikolazwa mama mkubwa wa Gervas aliyejitambulisha kwa jina la Martha Lugenge alisema kuwa vijana hawa walikutana Madibila kila mmoja akiwa katika shughuli zake ndipo walipoamua kuishi pamoja.
Alisema yeye alipewa taarifa za tukio hilo siku inayofuata na kwamba alipofika alikuta ndugu wa marehemu wameuchukua mwili wa mtoto wao kwa ajili ya taratibu za mazishi na kwamba hajui chanzo cha ugomvi uliosababisha wapigane visu.
Mama huyo alisema ''Wote ni watoto, kwani wameanza kuishi muda mrefu? wamekutana kila mmoja akiwa katika kazi zake, ndipo walipoanza kuishi kama mke na mume,''alisema



Zaidi ya watoto 60 wanadaiwa kutekwa na kufichwa katika handaki lililopo kwenye msitu wa Mabwepande, Wilaya ya Kinondoni , Dar es Salaam, ambalo ndani yake kuna jengo kubwa lenye vyumba.
Utekaji huo unadaiwa kufanywa na raia wa kigeni (Wazungu), wakishirikiana na Watanzania ambapo watoto hao hufungiwa katika vyumba hivyo, kuteswa, kulawitiwa na kubakwa.
Mtoto Emmanuel Robert (11) anayesoma darasa la tano Shule ya Msingi Maendeleo iliyopo Tabata, Segerea, Dar es Salaam na mdogo wake Godianus Robert (8), anayesoma darasa la tatu shuleni hapo, ndio waliofichua ukatili huo mwishoni mwa wiki.
Watoto hao walitekwa na Wazungu wawili asubuhi ya Septemba2 mwaka huu, wak ati wakienda shuleni na kufanikiwa

 kutoroka katika jingo hilo Septemba 23 mwaka huu.
Wakiwa wamechoka na afya zao kuzorota katika Kituo kidogo cha Polisi, Kibaha Maili Moja, mkoani Pwani, watoto hao walisema ndani ya jengo hilo kuna watoto wengi wa kike na kiume.
Walisema watoto hao wanafanyishwa kazi na kuteswa kwa kutandikwa fimbo, kuchomwa moto na kupigwa shoti ya umeme hasa wanapowaulizia wazazi wao ambapo baadhi yao hubakwa na kulawitiwa.
"Jumba hili limejengwa ndani ya handaki, tulikuwa tukifanyishwa kazi ngumu na nzito, usiku tunajaza maji katika mapipa mengi na kubebeshwa ndoo kupanda na kushuka kilima.
"Tunapigwa fimbo, wasichana wanafungiwa kwenye vyumba, wanabakwa na kulawitiwa kwa zamu na Wazungu, tunachomwa moto (alionesha mguu wake uliochomwa) na kupigwa shoti ya umeme tunapowaulizia wazazi wetu," alisema Emmanuel kwa uchungu akitokwa na machozi.
Aliongeza kuwa, asubuhi ya Novemba 23 mwaka huu, katika jengo hilo kulitokea kutokuelewana kati ya Wazungu na Waswahili ambapo mswahili mmoja aliwatisha wazungu kwa kuwaambia polisi wanakuja hivyo walikimbia na kuacha mlango wazi.
"Hali hiyo iliniwezesha mimi, mdogo wangu na watoto wengine wachache waliokuwa na nguvu kufanikiwa kutoroka, nilimshika mkono mdogo wangu ambaye alionekana kuchoka nikamvuta.
"Watoto wengine wachache waliokuwa na nguvu nao wakatoka, wengi hawakuweza kutoka kutokana na kukosa nguvu, wanaumwa, wana vidonda vikubwa mwilini kutokana na kuchomwa moto na kupigwa shoti ya umeme, wasichana hawakuweza kabisa kutoka kwa kuwa wamefungiwa ndani ya vyumba," alisema Emmanuel
Aliongeza kuwa , alijikokota taratibu na mdogo wake mbali ya maumivu makali waliyonayo akatokea Mswahili mmoja ambaye alikuwa na gari lenye vioo vyeusi akawaambia wapande ili awatoroshe.
"Tulipanda gari hilo akatushusha darajani mpakani mwa Manispaa ya Kinondoni na Wilaya ya Kibaha, jirani na mzani eneo ambalo sisi hatukuwa tukilifahamu...dereva huyo alituambia gari limeishiwa mafuta hivyo alitutaka tumsubiri aende kuyanunua.
"Tulitembea kidogo tukiwa hatujui tunakokwenda... tulikaa kando ya barabara kutokana na uchovu pamoja na njaa kali kwani katika jengo hilo mbali na kazi nzito tulizokuwa tukizifanya na mateso mengi, mlo ulikuwa mmoja tu kwa siku.
"Tulikula saa 10 jioni, wali na maharage...tukiwa kando ya barabara, nilisikia sauti ya baba yangu wa kufikia, dereva wa magari makubwa yanayobeba kokoto ikiniita.
"Nilidhani naota kumbe ilikuwa kweli, alikuja akatukumbatia akalia kwa uchungu kwa namna tulivyokuwa tumechoka na afya kuzorota, akatupeleka polisi ambapo tulipatiwa maji tukaoga na kupewa chakula kizuri na kitamu, tukala na kupata nguvu za kuzungumza vizuri," alisema Emmanuel.
Akizungumza na Majira, Emmanuel alisema baada ya kutekwa yeye na mdogo wake, walifungwa na vitambaa vyeusi usoni hadi walipofikishwa ndani ya jumba hilo la mateso.
Aliiomba Serikali kufanya jitihada za hali na mali ili kuwaokoa watoto wengine waliopo katika jengo hilo.
Mama mzazi wa watoto hao, Martha Godianus (29), ambaye anafanya shughuli za mama lishe, njia panda y a Ba r a k u d a , Ta b a t a Manispaa ya Ilala, alisema amehangaika zaidi ya miezi mitatu kuwatafuta watoto hao bila mafanikio.
"Nimepoteza fedha nyingi kwa kuwatafuta na kutapeliwa mara kadhaa katika kuhangaika," alisema Godianus huku akitokwa na machozi ya furaha katika Kituo kidogo cha Polisi Maili Moja.
Alisema zaidi ya watoto saba walipotea katika mtaa wao, wawili wakapatikana baada ya wiki mbili, wengine wakiwemo wanaye wakawa hawajapatikana na kuomba Serikali ilichukulie kwa uzito suala hilo ili kubaini kundi linalowateka watoto na kuwatesa.
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Ulrich Matei alikiri kutokea kwa tukio hilo na kuanza kulifanyia kazi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Dar es Salaam.
Alisema makachero wa polisi wamewahoji watoto hao ili kupata maelekezo ya kufika katika andaki hilo na kuwataka watu wote wenye taarifa za eneo hilo watoe ushirikiano.
MAJIRA

BINTI ALIYEKUWA AKISUBIRI MATOKEO YA KIDATO CHA NNE AUAWA NA MPENZI WAKE 

MWANAFUNZI aliyehitimu kidato cha nne mwaka huu, Sharifa Abdallah (18) ameuawa kwa kuchomwa kisu shingoni na mbavuni chumbani kwa mvulana aliyedai kuwa mpenzi wake maeneo ya Kimara Golani, Dar es Salaam.
Tukio hilo lilitokea majuzi saa 8:30 mchana na baadaye mvulana huyo aliyetambuliwa na Polisi kwa jina la Abdul Alpha (22) kujisalimisha katika kituo cha Polisi cha Stendi Kuu ya Mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo, akidai alikuwa akitaka kutoroka lakini aliona amefanya dhambi kubwa.
Akizungumza jana, mama mkubwa wa marehemu, Mwajuma Khamis alisema Sharifa alimaliza kidato cha nne
katika sekondari ya Luguruni na alikuwa akisubiri matokeo.
Alisema juzi waliporejea kutoka kazini hawakumkuta nyumbani, waliulizia kwa ndugu kutokana na kwamba hakuwa na tabia ya kutoka nyumbani, lakini hawakufanikiwa kumpata hadi jioni ndipo polisi walipowataarifu kupatikana kwa mwili wake.
Alisema mwili wa marehemu ulikutwa chumbani kwa kijana huyo karibu na nyumbani kwao ukiwa na majeraha mwilini, lakini hawakujua kama mtoto wao ana mwanaume, wanatarajia kumzika kesho saa saba mchana.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura alisema polisi walipata taarifa za tukio hilo katika kituo cha Ubungo na kwenda katika chumba cha kijana huyo kilichokuwa kimefungwa kwa ndani na kukuta mwili wa msichana huyo ukiwa umejeruhiwa.
Alisema baada ya kumhoji mtuhumiwa, alisema alifanya hivyo kutokana na wivu wa kimapenzi, kwani alikuwa na uhusiano na msichana huyo lakini wazazi wa msichana hawakutaka amwoe, hivyo kumtaarifu kuwa amepata mchumba mwingine.
Alipoulizwa kwa nini hakutoa taarifa katika kituo cha Polisi Kimara alikofanyia mauaji, alisema aliogopa watu wa maeneo yale wangempiga na kumwua, kwa kitendo hicho.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Tumbi, Kibaha, huku kijana huyo akishikiliwa na Polisi.


No comments: