Thursday, October 3, 2013

UEFA CHAMPIONS LEAGUE PELLEGRINI ASALIMU AMRI, ROBBEN ASEMA CITY NI WEPESI
BAADA ya Jana kumalizika kwa Mechi za Pili za Makundi ya UEFA CHAMPIONS LIGI, UCL, huku maneno makubwa yakiwa kipondo cha Bao 3-1 walichoshushiwa Manchester City Nyumbani kwao Etihad na Mabingwa wa Ulaya Bayern Munich na pia Wadau kuiona Man United ikitoka Sare ya Bao 1-1 Ugenini huko Donetsk, Nchini Ukraine, dimba ambalo Chelsea na Arsenal walikiona cha Mtema Kuni, yafuatayo ni maoni ya baadhi ya Wadau.
PELLEGRINI NA KICHAPO
Mabingwa Bayern Munich walitoa somo kubwa la Kandanda safi kwa kuichapa Man City Uwanja kwao Etihad Bao 3-1 katika Mechi ya Kundi D la UCL huku Bao hizo zikipigwa na Franck Ribery, Thomas Muller na Arjen Robben na City wakifunga Bao lao kupitia Alvaro Negredo.
Mechi hii ilishuhudia makosa makubwa ya Kipa wa Man City, Joe Hart, ambae ndie Kipa Nambari Wani wa England, na pia Kadi Nyekundu kwa Jerome Boateng wa Bayern.
Matokeo haya yamewafanya Bayern Munich wawe kileleni mwa Kundi D na kuwaacha Man City na CSKA Moscow kugombea Nafasi ya Pili.
Meneja wa Man City, Manuel Pellegrini, amekiri: “Tulicheza vibaya sana. Bayern, kama Siku zote, walicheza vizuri mno. Tumepata somo kubwa toka Magoli yao. Hatukuwa na nafasi tukiwa na Mpira miguuni kwetu.”
Pellegrini pia alikiri kukerwa na fomu ya Kipa wake Joe Hart na kusema: “Ni kweli nina wasiwasi na makosa lakini hiyo haikuwa Gemu rahisi!”
PEP GUARDIOLA
Pep Guardiola, Meneja wa Bayern Munich, alisema: “Nilisema Jana na sijabadilika. Man City wataingia Raundi ijayo na ni wapinzani wagumu kwa Timu yeyote. Tulicheza vizuri, tumeshinda na Soka ni spesho. Nina bahati kuwa na Wachezaji hawa. Ni safi kuja kwenye Nchi hii, wanayopenda sana Soka, na kucheza vizuri kama leo.”
ARJEN ROBBEN
Arjen Robben, ambae alifunga Bao moja kwa Timu yake Bayern Munich, alisema: "Tulitawala dhidi ya Timu kubwa Ulaya. Hatukutegemea Gemu nyepesi na rahisi kama ile!”
GARY NEVILLE
Gary Neville, ambae ni Kocha Msaidizi kwenye Timu ya Taifa ya England na pia Mchambuzi wa Soka kwenye Kituo cha TV cha SKY, mara baada ya Joe Hart kuruhusu Bao la Dakika ya 7 la Shuti la mbali la Franck RibĂ©ry, alisema: “Ni shuti la nguvu. Joe Hart alitakiwa kucheza vizuri zaidi, amefungwa kwenye Posti ya karibu yake, Mpira umempenya mikononi. Si mwanzo mzuri kwa Man City na Kipa.”
Baada ya Bao la Dakika ya 60 la Arjen Robben, Neville alisema: “Unaweza kusema Joe Hart alitakiwa kucheza vizuri tena. Amefungwa tena kwenye Posti ya karibu yake. Hii ni mara ya pili sasa. Lazima atahuzunika.”
MAN UNITED NA SARE
DANNY WELBECK
Danny Welbeck, ambae ndie aliefunga Bao walipotoka droo 1-1 na Shakhtar Donetsk huko Ukraine hapo Jana Usiku,  anaamini huu ni wakati wa Manchester United kuwa pamoja baada ya mwanzo mgumu kwa Meneja wao mpya David Moyes.
Sare hiyo imewafanya Man United wabaki kileleni mwa Kundi A la UCL wakiwa na Pointi 4 sawa na Shakhtar Donetsk lakini wao wako juu kwa ubora wa Magoli.
Moyes amekuwa kwenye presha baada ya Jumamosi iliyopita kufungwa Old Trafford na West Bromwich Albion Bao 1-0 kwenye Mechi ya Ligi Kuu England lakini Jana walicheza vizuri dhidi ya Timu ambayo haijapoteza kwao ikicheza na Timu za England na Jana Shakhtar walinusurika baada kusawazisha Bao Dakika 14 kabla Mpira kwisha kwa Bao la Taison.
Welbeck alinena: "Yalikuwa si matokeo mabaya. Sidhani kama kuna Timu nyingi zimekuja hapa na kupata Pointi 3. Pointi 4 kwa Mechi mbili si mbaya. Ni wazi sisi ni Manchester United na tunataka kushinda kila Gemu. Lakini kupata Pointi 1 hapa inaridhisha. Mambo hayendi vyema kwenye Ligi lakini lazima tuwe pamoja na kutilia mkazo Gemu yetu ijayo tu na si mbele.”
DAVID MOYES
Nae Meneja David Moyes, mara baada ya Mechi na Shakhtar, alizungumza: “Ni Pointi nzuri kwenye UCL kuipata hapa. Inabidi tushinde Gemu nyingine ili tusonge!”
Ukiondoa Sare ya Jana, Shakhtar walishinda Mechi zao zote 3 zilizopita kwenye UCL dhidi ya Klabu za England zilizochezwa Donetsk kwa kuzifunga Chelsea Msimu wa 2012/13 na Arsenal Misimu ya 2000/01 na 2010/11.
MIRCEA LUCESCU
Kocha wa Shakhtar Donetsk, Mircea Lucescu, Mkongwe wa Miaka 68 ambae yuko na Klabu hiyo tangu 2004, amekubali Sare ilikuwa Matokeo yanayoridhisha pale aliposema: “Tuliwaruhusu Man United kupata Bao la mapema na ilibidi tuhangaike kusawazisha. Sare hii ni Matokeo yanayoridhisha yanayofanya Klabu zote ziwe na nafasi nzuri kusonga.”
Man United sasa inakabiliwa na Mechi mbili mfululizo dhidi ya Real Sociedad ambao wako mkiani mwa Kundi A baada kuchapwa Mechi zao zote mbili dhidi ya Shakhtar na Bayer Leverkusen.

No comments: