Tuesday, October 8, 2013

KENYA YARUHUSIWA KUANDAA MICHUANO YA CHALLENGE
Mwenyekiti wa FKF Sam Nyamweya
KAMATI ya Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limetoa kibali kwa Kenya kuandaa michuano ya Senior Challenge Cup mwaka huu.
Katibu Mkuu wa CECAFA ameondoa wasi wasi wa awali kwamba michuano hiyo inaweza isifanyike nchini Kenya kutokana na mvutano kati yake na mwenyekiti wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF), Sam Nyamweya.
“Kwa hakika sivutani na Nyamweya. Ningependa kuwahakikishia Kenya kwamba mechi za Senior Challenge zitafanyika Kenya na tayari tumeanza kutafuta mdhamini mkuu,” alisema Musonye katika mkutano na waandishi wa habari.
Hata hivyo, Musonye alisema aliamua kuinyima Kenya nafasi hiyo mwaka uliopita, kwa lengo la kutaka zifanyike nchini mwaka huu taifa linaadhimisha miaka 50 tangu Kenya ipate uhuru.
“Nilikuwa na mawazo mazuri kwa sababu sasa yatakuwa mashindano ya hali ya juu kwa vile yataenda sambamba na sherehe za kuadhimisha miaka 50 za uhuru wa Kenya,” alisema.
“Itabidi hata Serikali itambue mashindano hayo,” aliongeza.
Nyamweya alisema kwa mara ya kwanza, uwanja wa Kenyatta Stadium mjini Machakos utaandaa baadhi ya mechi za mashindano hayo ya kimataifa.
Alisema ukarabati katika uwanja huo unaendelea ili uweze kukaliwa na mashabiki 8,000.
“Tunataka kupeleka boli mashinani na tumetambua Machakos kama mojawapo wa viwanja vitakavyotumika mwaka huu,” alisema Nyamweya.
Alisema viwanja vingine ni Kisumu Moi Stadium ambao utakuwa umekamilika kabla ya mechi hizo kuanza Novemba 27 na kuendelea hadi Desemba 12.
“Kadhalika kuna Mumias Complex na Afraha Stadium,” aliongeza.
Alisema tayari Magavana wa eneo hizo wamejumuishwa katika kamati andalizi wa michuano hiyo itakayoshirikisha timu 12.
Waliokuwa mabingwa wa Afrika, Zambia na Malawi zimealikwa kutoka nje ya jimbo la CECAFA.
Nyamweya alisema lengo la mashindano ya mwaka huu ni kuleta amani barani Afrika.
“Tunataka kutumia mashindano haya kuleta amani nchini Somalia. Tutafanya maandamano ya amani kabla ya mechi hizo kuanza,” alisema Nyamweya.
Rais wa CAF, Issa Hayatou anatarajiwa kuwa mgeni wa heshima wakati wa mashindano hayo.
Nchi 12 zilizothibitisha kushiriki ni wenyeji, Kenya, mabingwa watetezi Uganda, Tanzaania, Rwanda, Burundi, Ethiopia, Sudan Kusini, Sudan, Somalia, Eritrea, Djibouti na Zanzibar.
Kenya ilikuwa muandalizi kwa mara ya mwisho mnamo 2009.

No comments: