AJINYONGA BAADA YA KUMUUA MKEWE KWA UGOMVI WA KIMAPENZI
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Evaresti Mangala alisema Galawa alimuua mkewe Veronica Kashinje (25) kwa kumnyonga shingo na yeye kujitoa uhai kwa kujinyonga kwa kutumia kipande cha khanga nyumbani kwao kijijini hapo.
Alisema ofisini kwake kuwa, tukio hilo lilitokea saa moja usiku siku ya juma tatu katika kijiji hicho cha Idukilo Kata ya Mwadui Luhumbo, Tarafa ya Mondo wilayani Kishapu.
Alisema inadaiwa kuwa Galawa alikuwa na ugomvi wa mara kwa mara na mkewe kwa kumtuhumu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamume mwingine.
"Inadaiwa kuwa Veronica alifikwa na mkasa huo baada ya kuwa amerejea nyumbani akitoka kijijini kwa wazazi wake na haikuweza kufahamika kama kabla alikuwa ameondoka nyumbani kwake kutokana na ugomvi au la," alisema Kamanda Mangala.
Alisema mwili wa Galawa ulikutwa ukiwa unaning'inia juu ya dari kwenye kitanzi cha khanga na mwili wa mke wake ulikuwa umefungwa kamba shingoni na kufungwa kwenye mguu wa kitanda.
Alisema inawezekana kwamba baada ya jaribio la mwanamume huyo kujaribu kumbeba mke wake na kumning'iniza juu ya dari kushindikana, aliamua kumfunga kwenye kitanda ili ionekane na yeye amejinyonga.
Alisema hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na mauaji hayo na kwamba uchunguzi wa awali wa Polisi umebaini kuwa chanzo ni wivu wa mapenzi na wanandoa hao wameacha watoto watatu wenye umri kati ya miaka mitano na mitatu.
No comments:
Post a Comment