MIKOA YA LINDI NA MTWARA IMEKITHIRI KWA VITENDO VYA UKATILI NA UNYANYASAJI WA KIJINSIA, ILALA NDIO KINARA KILA SIKU WATOTO WATANO HUNAJISIWA
![]() |
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Valerie Msoka |
Taarifa ya Ofisa Elimu anayeshughulikia takwimu za shule za sekondari wilayani Newala, Magnus Munyuku, inaonyesha kuwa mwaka jana zaidi ya wanafunzi 30 walisimamishwa masomo kutokana na kupata mimba.
Takwimu hizo zilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Valerie Msoka, wakati wa uzinduzi wa ripoti ya matukio ya ukatili wa kijinsia.
Nayo halmashauri ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam imebainika kuwa kinara wa matukio ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, ambapo kila siku wastani wa watoto watano hunajisiwa.
Wilaya hiyo ilikuwa na makosa ya ubakaji 171 (Januari-Desemba 2012), Januari –Juni mwaka 2013 kulikuwa na makosa ya ubakaji 124, huku makosa ya kulawiti yaliyoripotiwa ni 48 (Januari-Desemba 2012) na Januari –Juni 2013 makosa ya kulawiti ni 40.
Msoka alisema kuwa walifanya utafiti Aprili mwaka huu katika wilaya 10 za Tanzania Bara na Visiwani, ambapo walibaini kuwapo kwa matukio mengi yasiyoripotiwa katika vyombo vya kisheria.
Alisema kuwa si kesi zote zinaripotiwa polisi kutokana na kuwapo kwa makubaliano baina ya watu wanaotendewa vitendo hivyo, hatua inayolazimu kumalizwa kifamilia.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Kamanda wa Polisi Ilala, Marietha Minangi, zilionyesha kuwa matukio ya upigaji wa wanawake ni 70 katika kipindi cha Januari – Desemba mwaka 2012, huku Januari-Juni 2013 yakiripotiwa matukio 60.
Alisema kwa mujibu wa Mratibu wa jinsia upande wa afya, Bertha Magasi, takwimu zilizopatikana kutoka Hospitali ya Amana kwa mwaka 2008 zilionyesha kuwa asilimia 55 ya wasichana na 23 ya wanawake walifika katika hospitali hiyo kutibiwa kutokana na kufanyiwa vitendo vya ubakaji.
Msoka alisema kuwa asilimia 21 ya wavulana na 24 ya wanaume walifika hospitalini hapo kutibiwa kutokana na kulawitiwa.
Msoka alisema kuwa tatizo la ubakaji limeonekana kuendelea kushamiri katika jamii ambapo takwimu zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2011 na mwaka huu, jumla ya kesi 341 za ubakaji zilitokea katika wilaya tatu za Wete, Unguja Kusini na Kusini Magharibi huko Zanzibar.
Alisema kuwa takwimu za kipolisi, shehia na ustawi wa jamii zilionyesha kuwa mwaka 2011 Wilaya ya Wete ilikuwa na matukio 22.
No comments:
Post a Comment