KENYA YAWASILISHA MSWADA WA KUDHIBITI UONGO KWENYE UHUSIANO
Bunge nchini Kenya lipo mbioni kupitisha mswada mpya wa ndoa ambao utaamuru kuwalipa fidia wale waliowadanganya kwenye mapenzi.
Kulingana na mswada huo utakaowasilisha bungeni Jumanne alasiri, mahakama inaweza kuagiza anayevunja ahadi ya kumwoa mwingine amlipe ikiridhika kwamba jambo hilo lilimuathiri kwa njia moja ama nyingine
Mswada huo unalenga kuunganisha sheria saba zilizoko kwa sasa kuhusu ndoa, talaka na masuala mengine kuhusu ndoa kati ya mwanaume na mwanamke.
Ukipitishwa, ndoa za wake wengi na kulipa mahari kwa njia ya kitamanduni zitatambuliwa rasmi kisheria.
Kifungu kuhusu kutotimiza ahadi ya kuoana kinasema ingawa ahadi hiyo haifungi mtu kisheria na sio lazima aoe anayemuahidi, ahadi hiyo inaweza kubadilika kuwa deni.
Kulingana na Wakili Grace Maingi, sehemu hii sio kali kama inavyooneka kwa sababu mahakama ndiyo itaamua iwapo kuna fidia yoyote inayopasa kulipwa aliyeachwa na mchumba wake.
Mswada huo haufafanui maana ya ahadi ya kuoana na hivyo kuachia mahakama jukumu hilo.
Bi Maingi alisema mswada huo utasaidia kulinda ndoa kulingana na katiba.
Mwenyekiti wa Shirika la Wanawake Mawakili Nchini, FIDA Bi Ruth Aura, alisema mswada huo utasaidia kushughulikia mambo ambayo hayakuwa katika sheria za awali.
Alisema mswada huo utawalinda wajane dhidi ya dhuluma za mashemeji kwa sababu vyeti vitatolewa kwa kila aina ya ndoa.
Alisema sehemu inayosema kila mke katika ndoa ya wanawake wengi anapasa kuwa na cheti cha ndoa itafanya kila mmoja kuhisi salama katika ndoa.
Mswada huo unafafanua kwamba ndoa ni kati ya watu wa jinsia tofauti na hivyo wanaolenga kuhalalisha ndoa za jinsia moja watapata pigo.
Ukipitishwa, wanaooa watu wa familia zao watakuwa wakishiriki tendo la uhalifu.
Wachumba pia watakuwa na hiari ya kuamua ikiwa ndoa yao itakuwa ya mke mmoja kumaanisha ni makosa kujaribu kuoa mke mwingine baadaye.
Katika hali hii, kila mmoja atatakiwa kutangaza nia yake mbele ya afisa wa kusimamia ndoa, kuandika na kutia saini akiapa kutimiza aliyoamua.

No comments:
Post a Comment