Monday, July 8, 2013

BADO WANAUME WENGI WANANYANYASWA NA WAKE
 ZAO NCHINI KENYA

WANAUME wengi nchini Kenya wanapigwa na wake zao lakini hawaripoti visa hivyo kwa kuogopa aibu.
Kulingana na mshirikishi wa kitaifa wa shirika la kutetea wanaume la MenKen, Bw Fredrick Nyaga, wanaume ndio wanaoathiriwa zaidi na dhuluma za kinyumba hata kuliko wanawake.
“Katika visa vyote vya dhuluma za jinsia, ni chini ya asilimia tatu pekee iliyoripotiwa miongoni mwa wanaume ambao wamedhulumiwa na wanawake. Hii ni kutokana na wanaume kunyamaza kwa aibu,” amesema.
Bw Nyaga alikuwa akizungumza kwenye hafla ya kuzinduliwa kwa ripoti ya sera kuhusu kushirikisha wanaume katika juhudi za kuzuia uambukizaji Ukimwi na dhuluma za kijinsia katika mkahawa wa Sarova Panafric, Nairobi.
Ripoti hiyo iliyoandaliwa na shirika la MenKen kwa ushirikiano na mashirika ya kimataifa, inakosoa udhaifu uliopo kwenye sheria kwa sasa, ambao hauzungumzii kwa uzito suala la kudhulumiwa kwa wanaume pamoja na watoto wa kiume.
Alitoa wito kwa wanaume na wavulana washiriki bila kulegeza kamba katika masuala ya afya ya jamii na kuwajibika kama wazazi.
Katika hotuba yake, mshirikishi wa kitaifa katika mradi wa kupambana na dhuluma za kijinsia, Bi Itumeleng Komanyane, alisema mila, tamanduni na desturi za Kiafrika huchangia kwa kiasi kikubwa katika masuala ya jamii.
Alidai kuwa wanaume hulaumiwa zaidi kuliko wanawake katika ndoa nyingi.


No comments: