Friday, June 7, 2013

AHUKUMIWA KWA KUBAKA NA KUMPA UJAUZITO MWANAFUNZI



MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Musoma, imemhukumu kifungo cha miaka 35 na kuchapwa viboko 24, Mbogo Nashoni (19) mkazi wa Nyakato, baada ya kupatikana na hatia ya makosa mawili ya kubaka na kumpatia ujauzito mwanafunzi wa kidato cha kwanza (jina tunalo). Mahakama hiyo, pia imemuamuru mtuhumiwa kumlipa fidia mhanga huyo Sh milioni moja, baada ya kumaliza kutumikia adhabu yake.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Richard Maganga, ilidaiwa na mwendesha mashitaka wa Serikali, Jonas Kaijage Machi, 2012 muda usiojulikana, mshitakiwa alitenda kosa la kwanza la kubaka kinyume cha kifungu namba 130, kifungu kidogo cha kwanza na kifungu namba 131 kifungu kidogo cha adhabu cha Sheria Sura ya 16, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Kosa la pili, ni kumpatia mimba mwanafunzi kinyume cha sheria ya elimu, inayomzuia mwanafunzi kupata ujauzito kutokana na kifungu namba GN 265 ya mwaka 2003.
Mwendesha mashitaka, aliitaka mahakama kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ubakaji na kuwapatia ujauzito wanafunzi, ili iwe fundisho kwa watu wenye tabia kama hizo.

“Mheshimiwa hakimu, naiomba mahakama yako tukufu kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hii ya kuharibu maisha ya watoto wadogo hasa wanafunzi wa shule,” aliomba Kaijage.
Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, alidai baada ya kupitia mwenendo wa kesi aliridhika pasipo na shaka mshitakiwa alitenda makosa hayo kinyume cha sheria, hivyo kuamua kutoa adhabu kifungo cha miaka 30 na viboko 24 kwa kosa la kubaka.

Na kifungo cha miaka mitano kwa kosa la kumpatia mimba mwanafunzi, huku adhabu zote zikienda pamoja na kumpa fidia ya milioni moja, baada ya kumaliza kifungo chake.

Mtanzania.

No comments: