Thursday, May 16, 2013

TAIFA STARS YAJITOA COSAFA.



TIMU ya taifa ya soka ya Tanzania,Taifa Stars imejitoa kwenye michuano ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika-COSAFA itakayofanyika nchini Zambia kuanzia Julai 2 mpaka 26 mwaka huu.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka nchini,TFF, Angetile Osiah amesema Stars ambayo iliingizwa katika michuano hiyo kama timu mwalikwa imejitoa kutokana na mwingiliano wa ratiba kati ya michuano hiyo na mechi za Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani-CHAN. Amesema awali Tanzania ilithibitisha kushiriki michuano kwa matarajio kwamba Uganda ingekubali ombi la TFF la kubadilisha ratiba ya mechi za CHAN, lakini Shirikisho la Mpira wa Miguu Uganda,FUFA likagoma kwa vile kipindi ambacho kilipendekezwa lenyewe litakuwa na uchaguzi wa viongozi wao. Taifa Stars itacheza na Uganda, The Cranes katika mechi za CHAN ambapo mechi ya kwanza itachezwa jijini Dar es Salaam kati ya Julai 12-14 mwaka huu wakati ya marudiano itafanyika jijini Kampala kati ya Julai 26-28 mwaka huu. Akizungumzia michuano ya COSAFA, Kocha Kim amesema angependa kushiriki michuano hiyo kwani ingekuwa kipimo kizuri kwa kikosi chake, lakini kwa sasa malengo makubwa ya Stars kwenye mechi za mchujo za Kombe la Dunia na michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ambayo fainali zake zitafanyika mwaka 2015.

TIKETI SIMBA, YANGA KUANZA KUUZWA KESHO.

Tiketi kwa ajili ya pambano la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Yanga litakalochezwa keshokutwa (Jumamosi) kwenye Uwanja wa Taifa zitaanza kuuzwa kesho (Ijumaa) kwenye vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam. Vituo vitakavyouza tiketi hizo kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 10 jioni ni Uwanja wa Taifa, mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa Ohio na Samora, Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, OilCom Ubungo, kituo cha mafuta Buguruni, BMM Barbershop Sinza Madukani, Dar Live Mbagala na Sokoni Kariakoo. Tiketi hizo zitakuwa zikiuzwa katika magari maalumu yaliyoegeshwa katika vituo hivyo. Viingilio katika mechi hiyo ya kufunga msimu ni sh. 5,000 kwa viti vya kijani, sh. 7,000 viti vya bluu, sh. 10,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 VIP C, sh. 20,000 VIP B n ash. 30,000 kwa VIP A.



No comments: