Monday, April 1, 2013

MAREKEBISHO YA SHERIA YA NDOA YAJA


Angela Kairuki naibu waziri wa katiba

Na Asha Bani

NAIBU Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki amesema ni wakati muafaka wa kusimamia marekebisho ya sheria ya mtoto wa kike na masuala ya ndoa.

Akizungumza jijini Dar es salaam jana Kairuki amesema mtoto wa kike kuozeshwa akiwa katika umri mdogo si tu ni ukiukwaji wa haki za binadamu bali pia kunahatarisha maisha yake.

Alisema serikali inatambua watoto wengi wa kike wamekuwa wakiolewa chini ya umri uliowekwa na sheria na mara zote hatua za kisheria zimekuwa zikichukuliwa dhidi ya wazazi, walezi, na wanaume wanaowaoa wasichana hao.

Alisema kwa kutambua hilo kumekuwa na mijadala mingi juu ya umri wa mtoto wa kike kuolewa ambapo serikali inatambua matatizo yanayoweza kutokea iwapo mtoto huyo ataolewa kabla ya kutimiza umri stahiki.

Aidha, alisema serikali ina nia ya dhati ya kuifanyia marekebisho sheria ya ndoa kwa kuandaa waraka kwa ajili ya kukusanya maoni kutoka kwa wananchi yatakayowezesha sheria hiyo kubadilishwa ili kukidhi mahitaji.

Aidha atahakikisha anasukuma mchakato wa kuzifanyia marekebisho Sheria ya Urithi, Sheria ya Ndoa na kuzifanyia mapitio sheria nyingine mbalimbali, ili kutokomeza unyanyasaji na ukatili wa kijinsia na kingono kwa wanawake na watoto hususan wasichana.

“Pia serikali itaangalia namna ya kuzifanyia mapitio Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ya Mwaka 1998 na Sheria zingine kama Sheria ya Ardhi ambazo zinaweza kutoa fursa zaidi na kuwalinda wanawake, wasichana na watoto ili waondokane na unyanyasaji,” alisema Kairuki.

Tanzania daima

No comments: