Friday, March 8, 2013


siku ya wanawake iwahusishe wanawake wa kada zote

 
Na Elizabeth Mjatta
LEO ni Siku ya Wanawake Duniani, ambapo wanawake wa Tanzania huungana na wanawake wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa duniani kote kuadhimisha siku hii. Maudhui makubwa ya siku hii ni kutoa fursa ya kupima utekelezaji wa maazimio, matamko na mikataba mbalimbali ya kimataifa na kitaifa kuhusu masuala ya maendeleo ya wanawake katika nchi yao.
Madhumuni mengine mahususi ni kujenga mshikamano wa wanawake duniani kote, kuhamasisha jamii kushiriki kutatua changamoto zinazowakabili wanawake kwa kuzingatia kauli mbiu ya maadhimisho ya kila mwaka.

Siku hii ni ya kipekee kwa wanawake wa kada mbalimbali kukutana na kufanya shughuli mbalimbali, ikiwemo kuendesha mijadala, kufanya mikutano ya hadhara, yote yakiwa na lengo la kujumuika kwa pamoja kujadili masuala yao.

Lengo na maudhui ya siku hii yanawagusa wanawake wote, kiasi kinachotia faraja kwa kila mwanamke mpenda maendeleo.

Lakini wakati maudhui na malengo ya siku hii yakiwagusa wanawake wote, yapo malalamiko kuwa kundi kubwa la wanawake wasionacho wanaachwa nyuma.

Wanawake hao wanadai kuwa siku hii imetekwa na wanawake wachache ambao wanajulikana au kuwa viongozi katika maeneo fulani.
Hoja hii inaweza ikawa na mashiko au isiwe na mashiko, lakini ni vyema ikaangaliwa na kufanyiwa kazi kwa uzito wake, kwani waswahili wanasema lisemwalo lipo na kama halipo basi linakuja.

Jambo jingine ni kuwa wakati siku hii inaadhimishwa, lipo kundi la wanawake ambao hawajui uwepo wa siku hii, lengo lake na maudhui kwa ujumla.

Hili nalo linatia shaka na linaweza kutia mashiko ya ile shaka ya mwanzo kwamba siku hii iko kwa ajili ya wanawake fulani.

Ndiyo. Nasema hivi kwa sababu kupitia kazi yangu nimejaribu kuwadodosa baadhi ya kinamama, hususan wanaojishughulisha na biashara ndogondogo na wale kinamama wasio na ajira, maarufu kama mama wa nyumbani, wengi wa kundi hili majibu yao ni kuwa “ mimi mbona sijui”, “aah hiyo itakuwa siku ya wanawake wakubwa au viongozi”.

Nilipowauliza kuwa kwani hawajasikia katika vyombo vya habari? Walijibu “hata kama ukisikia lakini kitu hukijui kwa undani wake utaelewa nini, kama ingekuwa ni kwa wanawake wote si tungeona watu wanapita kutuhamasisha.

“Mbona mambo mengine, ikiwemo uchaguzi watu wanatuhamasisha mpaka mitaani mwetu, iweje hii siku ya wanawake? Mi naona kuna wanawake maalum na siyo sisi wa majumbani”.

Ukiangalia kwa makini kauli hizi, zinatoa picha halisi ya jambo hili kwamba inaonekana kabisa kuna kundi limeachwa nyuma, inawezekana umuhimu wa siku hii na namna ya wanawake kushiriki haujawekwa wazi sana na ndiyo maana kuna kundi linalalamika kuachwa.

Ndiyo, nasema hivyo kwa sababu malalamiko haya siyo ya leo, bali yamekuwepo kila mwaka na sijui kama wahusika wamekuwa wakisikia kilio hiki na kukifanyia kazi.

Ukiacha wanawake walio mijini, wapo pia wa vijijini ambao nina uhakika hawajui kuhusu siku hii, ndiyo maana nasema ipo haja ya wizara husika kufanya mikakati ili siku hii ijulikane Tanzania nzima na si katika mikoa michache.

Ni vyema wizara husika ikaweka mkakati wa kuwafikia wanawake wengi zaidi, ikajiwekea malengo ya kufuata makundi maalum na kutoa elimu juu ya ushiriki wao katika siku hii.

Lakini kingine wakati tunasherehekea siku hii, ni vyema iwepo mikakati ya kuhakikisha masuala ya ukatili wa kijinsia yanapewa kipaumbele, ikiwemo kuweka mada na mijadala katika vyombo mbalimbali vya habari.

Kwa sababu yapo matukio mengi ya wanawake kubakwa, kulawitiwa na kuuawa.

Kwa mwaka huu tumesikia na kushuhudia matukio mengi ya kutisha waliyofanyiwa wanawake, baadhi yao wameuawa kinyama, kati yao wapo waliouawa na waume zao.
Mambo haya hayaleti picha kwamba ipo siku moja masuala ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake yatamalizika, nasema hivyo kwa sababu yamekuwa yakijirudia kila mara, hali inayomfanya mwanamke kuendelea kuwa mnyonge.

Naamini kabisa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ndiyo wahusika wakuu wa shughuli hii, hebu wajipambanue na kuifanya shughuli hii iwahusishe wanawake wengi zaidi.

Wafanye hamasa kuanzia ngazi ya kata, kijiji, wilaya hadi mkoa, ili kuwavuta wanawake wengi zaidi kuelewa umuhimu wa siku hii.
Naamini wakiamua kuweka kampeni maalum wanaweza, kwani huko wataweza kupata maoni mbalimbali ya jinsi ya kumsaidia mwanamke kuondokana na masuala ya ukatili wa kijinsia.

Kuelewa mikataba ya kitaifa inayomhusu mwanamke, lakini kuelewa kwa kina haki zao za msingi.

Shime wanawake tusherehekee siku hii kwa kutambua wajibu wetu kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.

Mungu Ibariki Tanzania.
Mungu wabariki Wanawake Wote.

No comments: