TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO
TENGA AKEMEA VIJEBA COPA COCA COLA
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
Leodegar Tenga amewataka viongozi wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa
kuhakikisha wanaingiza wachezaji wenye umri sahihi katika michuano ya U15 FIFA
Copa Coca-Cola 2013.
Ametoa mwito huo leo (Machi 26 mwaka huu) wakati
akifungua semina elekezi ya michuano ya Copa Coca-Cola ambayo kuanzia mwaka huu
itakuwa ikishirikisha watoto wenye umri chini ya miaka 15.
Rais Tenga amesema hakuna jambo la kipuuzi kama
kuchomekea wachezaji ambao wamezidi umri unaotakiwa kwa vile lengo la michuano
ya aina hiyo ni kubaini vipaji na kuwafanya watoto wapende kucheza mpira wa
miguu.
“Kwanza nawashukuru kwa kutenga muda wenu na
kuhudhuria semina. Lakini ni vizuri pia mkahakikisha mnakuwepo kwenye mashindano
ili kutekeleza haya ambayo tutakubaliana katika semina hii. Mkileta mtu
mwingine anaweza kutuanzishia mambo mengine badala ya yale tutakayokubaliana,”
amesema Tenga.
Pia ameishukuru kampuni ya Coca-Cola ambaye imekuwa
ikidhamini michuano hiyo tangu mwaka 2007 ambapo semina hiyo elekezi
inayoshirikisha makatibu wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa na waratibu wa
mikoa wa michezo ya UMISSETA ni ya saba mfululizo.
Ratiba ya michuano hiyo kuanzia mwaka huu
imebadilika ambapo sasa itaanzia ngazi ya wilaya Aprili wakati fainali katika
ngazi ya Taifa itachezwa Septemba.
SIMBA, KAGERA SUGAR KUPAMBANA VPL
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania inaendelea kesho (Machi 27 mwaka huu) kwa mechi mbili ambapo bingwa mtetezi Simba atakuwa mgeni ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. Uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 3,000 unatarajiwa kushuhudia mechi yenye ushindini kutokana na uwezo wa wachezaji wa pande zote mbili.
Mechi
nyingine itapigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam
kati ya wenyeji Azam na Tanzania Prisons kutoka Mbeya.

No comments:
Post a Comment