Tuesday, March 19, 2013

KIONGOZI MPYA WA KANISA KATOLIKI AAPISHWA



Zaidi ya viongozi 130 kutoka nchi za nje,wafalme sita,viongozi zaidi ya 30 wa taifa na serikali akiwemo kansela Angela Merkel na makamo wa rais wa Marekani Joe Biden na viongozi wa kidini Wawakilishi wa dini ya kiyahudi na kiislam na wale wa kiorthodox wamehudhuria misa ya kuapishwa Papa Francis wa kwanza katika uwanja wa mtakatifu Petrus mjini Roma.
Baada ya kuvikwa skola na pete kuashiria sasa amekuwa kiongozi wa 266 wa kanisa katoliki ulimwenguni,Papa Francis wa kwanza alisema "madaraka ya kweli ya Papa ni huduma za dhati na unyenyekevu"

Papa Francis wa kwanza amesema Papa anabidi anyoshe mikono yake kwa ulimwengu mzima na hasa kwa wanyonge,watu walio masikini na dhaifu."

Akivalia joho jeupe na skola ya rangi hiyo hiyo huku akitabasamu,Papa huyo wa kwanza wa kutoka bara la Amerika aliingia katika uwanja wa Mtakatifu Petrus akiwa ndani ya gari lisilokuwa na paa,akishangiriwa kwa matarumbeta na shangwe za malaki ya waumini huku bendera za ulimwengu mzima zilipepea katika uwanja huo.

Baada ya kuuzunguka uwanja wa mtakatifu Petrus Papa Francis wa kwanza akifuatana na makadinali wa kanisa la kikatoliki, alikwenda kusali katika kanisa la muasisi wa kanisa katoliki.

Papa Francis wa kwanza aliyeachana na mtindo wa kupanda gari la viyoo vya kinga,alisimamisha kwa muda gari yake na kuteremka ili kumbariki bwana mmoja mlemavu.



No comments: