Tuesday, March 19, 2013

HII NAYO KALI; DIWANI AWACHAPA VIBOKO MUME NA MKE



DIWANI wa Bwanjai wilayani Misenyi, mkoani Kagera, Dickson Dismas (CCM), anadaiwa kuwachapa viboko Audax Nkoko na mkewe Domina kutokana na kutowakuta nyumbani kwao ambako alikwenda kuwapelekea fedha ili wakamfanyie kazi shambani kwake.

Akizungumza na Tanzania Daima, Nkoko ambaye ni mkazi wa kijiji cha Buhanga Ruti alisema tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki nyumbani kwake ambako diwani huyo alikwenda na sh 5,000 ili kuwapelekea kwa ajili ya kufanya shughuli hiyo.

Kwa mujibu wa Nkoko waliporejea nyumbani diwani huyo naye alikwenda kwa mara nyingine na kuwachapa viboko 10 kila mmoja huku akishuhudiwa na watoto wake na wanakijiji.

Baadhi ya wanakijiji walioshuhudia tukio hilo akiwamo Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kashekulo, Bazili Didas, alikiri kutokea kwake na kueleza kwamba diwani huyo alishawahi kumchapa mwanakijiji mwingine aliyemtaja kwa jina la Bubewa Kikutu.

“Hii si mara ya kwanza kwa mheshimiwa diwani kuwachapa viboko Audax na mkewe, kwani hivi karibuni alimchapa Kikutu kwa kosa ambalo halistahili kuadhibu kwa viboko tumefadhaishwa na jambo hili,” alisema Didas.

Alipotafutwa kwa njia ya simu naye Mbunge wa Nkenge, Assumpter Mshama, alipoulizwa kuhusu madai hayo alisema hayafahamu na kueleza kwamba kama kweli limetokea ni jambo lisilotakiwa ambalo linapaswa kuchukuliwa hatua na mkuu wa wilaya ya Misenyi.

“Mara nyingi nimekuwa nikipata malalamiko ya wananchi wa kata ya Bwanjai wakifanyiwa ubaya na Dismas, kwa hili la kujichukulia madaraka ya kisheria mkononi na kuwachapa mume na mke linapaswa kuchukuliwa hatua zaidi,” alisema Mshama.

Viongozi wengine waliochukizwa na tukio hilo na kuahidi kulitafutia ufumbuzi ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Buhanga, Johansen Kamala, pamoja na Mtendaji Kata wa Buhangaruti Albogasti Michael.

Chanzo: Tanzania daima

No comments: