Thursday, February 21, 2013

TBL YAKABIDHI BASI KWA TIMU YA TAIFA YA TANZANIA, TAIFA STARS



Na Prince Akbar
KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya Kilimanjaro, leo hii imekabidhi basi jipya kwa Timu ya Taifa (Taifa Stars), likiwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni 200 kwa udhamini wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager.

Hafla ya makabidhiano imefanyika Makao Makuu ya TBL jijini Dar es Salaam na kupewa Baraka na Mkurugenzi Mkuu wa TBL, Robin Goetzsche. Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na maofisa kutoka TFF, wafanyakazi za TBL, wadau wa soka na vyombo mbalimbali vya habari.

TBL imenunua basi hilo ikiwa ni sehemu ya ufadhili kama ilivyoanishwa katika mkataba baina ya pande hizo mbili. Mkataba huo ulitiwa saini Mei mwaka jana na lengo kuu ni kuinua kiwango cha Taifa Stars.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TBL alisema, kukabidhi kwa basi hilo ni ishara kwamba TBL itaendelea kuisadia timu ya taifa na hivyo kupandisha kiwango cha soka nchini na aliwataka wahusika kulitunza basi hilo kwa manufaa ya timu na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe alisema basi hilo lenye uwezo wa kubeba abiria 51, limenunuliwa kutoka Yutong na thamani yake ni zaidi ya Sh milioni 200.

Baada ya makabidhiano hayo, basi lilifanya ziara katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam ili mashabiki walione na kupiga picha huku kukiwa na matukio kadhaa ya kusisimua kama vile kucheza na kuimba.

Naye Rais wa TFF, Leodgar Tenga aliipongeza TBL kwa udhamini wake wa uhakika na kusisitiz akuwa tangu wameanza wameshatekeleza ahadi walizoahidi na moja wapo ikiwa ni kuhakikisha basi jipya linanunuliwa.

Bia ya Kilimanjaro ilianza kuifadhili Taifa Stars Mei mwaka jana kwa mkataba uliogharimu zaidi ya Sh bilioni 2 kwa mwaka katika kipindi cha miaka mitano na TFF.

No comments: