Tuesday, February 12, 2013

TASWA YAFUTA MDAHALO WA WAGOMBEA TFF.
Amiri Mhando

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kimefuta wazo la kuendesha mdahalo kwa wagombea wa nafasi za juu za uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Mdahalo huo ulikuwa ufanyike Februari 15, 2013 na tayari chama kilikuwa katika hatua nzuri ya mazungumzo na wadhamini pamoja na kituo kimoja cha televisheni kwa ajili ya kurusha 'live' tukio hilo, ambapo kesho ilikuwa tutangaze utaratibu mzima wa mdahalo huo.

Katika mazungumzo ya leo na uongozi wa kituo hicho ambao hautaki kukitangaze, wamekubaliana kufuta wazo la mdahalo kwa sababu nafasi ya urais amebaki mgombea mmoja, hivyo mdahalo hautakuwa na tija. Dhamira ya awali ya kufanya mdahalo ilikuwa kuwapa fursa wapiga kura wasikie vyema sera za wagombea urais na Makamu wa Rais, ili wananchi wawasikilize wagombea hao na pia wapiga kura wawatambue vizuri. Hata hivyo TASWA itatafuta utaratibu mwingine mzuri ambao utawezesha wagombea kuzungumza na waandishi wa habari na kuulizwa maswali mbalimbali ambayo tunaamini kwa kiasi fulani yatasaidia wapiga kura katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Februari 24 mwaka huu. TASWA inawatakia kila la kheri wagombea wote wa TFF waliobakia. TASWA imekuwa ikifanya mdahalo kwa wagombea wa nafasi za juu kwenye uchaguzi wa TFF, ilifanya hivyo mwaka 2001 na mwaka 2004 ingawa haukuwa wa live, ikafanya wa live mwaka 2008, ambapo yote ilikuwa ya mafanikio makubwa.

UCHAGUZI TFF WAPIGWA 'STOP', TENGA KUENDELEA KUPETA KARUME


TAARIFA KWA UMMA



UCHAGUZI WA VIONGOZI WA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA NA TANZANIA PREMIER LEAGUE BOARD (TPL)



KUSITISHA ZOEZI LA KAMPENI

12/02/2013



1. Kamati ya Uchaguzi, kwa mamlaka iliyonayo kupitia Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 3(1), 6(1) (g) na (l), 10(5), 11(6) inayosomeka pamoja na Ibara ya 14(1) na (2) na pia Ibara ya 26(5) na (6), imesitisha zoezi la kampeni za uchaguzi wa TFF na TPL Board lililokuwa lianze kesho tarehe 13/02/2013 hadi hapo itakapowatangazia, ili kuhakikisha kuwa mchakato wa uchaguzi unakidhi kikamilifu matakwa ya Kanuni za Uchaguzi na Katiba ya TFF.



2. Tarehe za Uchaguzi Mkuu wa TFF na TPL Board zinabaki kama zilivyopangwa.



3. Taarifa hii inazingatia pia Ibara ya 2(4) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF inayoagiza uongozi uliopo madarakani kuendelea na kutekeleza majukumu ya Shirikisho hadi hapo mchakato wa uchaguzi utakapokamilika.



Deogratias Lyatto

MWENYEKITI

KAMATI YA UCHAGUZI TFF

WAJITOKEZA KUMTETEA MALINZI WAKIWA TAYARI KUFUNGUA KESI MAHAKAMANI KUZUIA UCHAGUZI TFF

Na Dina Ismail

WANACHAMA na mashabiki wa soka nchini wameapa kuandamana na kwenda Mahakamani kuzuia kufanyika kwa uchaguzi wa viongozi wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), baada ya Kamati ya Rufaa ya Shirikisho hilo kumuengua mgombea wa nafasi ya urais, Jamal Emil Malinzi.

Aidha, wanachama hao kutoka klabu za Simba, Yanga na Azam wamemtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete kuingilia kati suala la kuenguliwa kwa Malinzi kwani limefanywa kwa chuki binafsi likiwa na lengo la kumbemba mpinzani wake, Athumani Jumanne Nyamlani.

Wakizungumza na Waandishi wa habari leo, pamoja na kupinga kuondolewa kwa Malinzi, wametoa siku tatu kwa TFF kumrejesha katika kinyang’anyiro hicho, kinyume na hapo watakwenda kudai haki yao Mahakamani.

Mmoja ya wadau hao Kaisi Edwin alisema kwamba kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) chombo cha mwisho cha maamuzi ni Mahakama yas Usuluhishi wa Migogoro ya Michezo (CAS) lakini TFF haijaelekeza baada ya kamati ya Rufaa chombo kipi kinaweza kutoa suluhu ya masuala kama hayo.

Alisema walitaka kupata changamoto mpya ya uongozi kupitia kwa Malinzi lakiini kitendo cha kumuengua kunaonesha ni jinsi gani wanavyotaka kuendelea kuwa na watu wasiotaka maendeleo ya soka.

“Ni bora tufungiwe na FIFA, tunajua maslahi wanayoyapata TFF na tutatoa uozo wote...kwa hili hata damu itamwagika na kwa gharama yoyote tutahakikisha uchaguzi haufanyiki kama wasipomrejesha Malinzi labda waende kufanyia Geneva,”aliusema Kaisi.

Naye Suleiman Kato alisema anashangazwa na kamati ya Rufaa kumuengua Malinzi kwa madai ya kutokuwa na uzoezfu wakati alipitishwa kugombea uchaguzi wa mwaka 2008 inagawa alishindwa kwa kura chache na rais wa sasa wa TFF, Leodger Tenga.

“Malinzi pia nia mwenyekiti wa chama cha soka Kagera sasa iweje apitishe kugombea huko na mpaka anapata kiti hicho nah ii leo mseme hana uzoefu na uongozi wa soka, kinachoonekana hapa ni kutaka kudidimiza soka la Tanzania, hilo hatulikubali,”alisema.

Mdau mwingine, Mgeni Ramadhan ‘Dogo Macho’ alisema inaonesha wazi wazi wanataka viongozi kwa ajili ya maslahi binafsi kitu ambacho si sahihi kwani Watanzania wanaopenda soka wanataka maendeleo na si viongozi maslahi.

“Naamini Rais Kikwete ambaye ni mpenda michezo atasikia kilio hiki na kuingilia kati, kuna watu wapo kwa ajili ya kubebwa, huyo Nyamlani anatoka Kusini, kuna mwanakamati mmoja Murtaza mangungu ambaye ni Mbunge anambeba, pia kuna mwingine aliwahi kuwa Hakimu wa Temeke na nyamlani akiwa karani wake,”alisema.

Kwa upande wake, mdau mwingine Said Bakari alisema kuwa wataanza kuonesha hasira zao kuanzia leo kwenye uwanja wa Taifa kwenye mechi baina ya Yanga na African Lyon, kabla ya kuendelea na hatua yao katika michezo ya kimataifa ya timu za Simba na Azam wikiendi hii.

“Huyu Nyamlani anabebwa, kwani tunajua Mwenyekiti wa Kamati alikuwa rafiki yake wakati akiwa Hakimu Temeke yeye, alikuwa karani, Mangungu naye pamoja na kumpigia debe ni jirani na baba yake Nyamlani,”alisema.

Wadau hao kwa pamoja wamepaza sauti hizo baada kamati ya Rufaa ya TFF kumuengua Malinzi katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Februari 24 mwaka huu ambapo kwa mujibu wa ratiba kampeni zinatarajiwa kuanza leo.

Katika hatua nyingine, Malinzi kesho anatarajiwa kuzungunmza na waandishi wa habari kuhusina na sakata hilo.



UCHAGUZI TAFCA FEB 14


Na Boniface Wambura

UCHAGUZI wa viongozi wa Chama cha Waamuzi wa Soka Tanzania (FRAT) unafanyika Februari 14 mwaka huu mjini Morogoro kama ulivyopangwa, tofauti na taarifa wanazopewa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho.

Kwa mujibu wa Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ya FRAT, Damas Ndumbaro, wajumbe wa Mkutano Mkuu wa FRAT wanatakiwa kufika Morogoro keshokutwa (Februari 12 mwaka huu) . Pia wapiga kura na wagombea wanatakiwa kulipia ada za uanachama kwa mwaka 2013 kabla ya uchaguzi.

Wagombea ni Army Sentimea na Said Nassoro (uenyekiti) wakati wanaoomba nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni Juma Chaponda, Juma Mpuya na Tifika Kambimtoni.

Abdallah Mitole, Charles Ndagala na Hamis Kisiwa wanawania ukatibu mkuu, nafasi ya Mhazini inagombewa na Jovin Ndimbo. Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni Kamwaga Tambwe wakati nafasi ya uwakilishi wanawake yupo Isabela Kapera.

Wagombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Emmanuel Chaula na Samson Mkotya



TFF YATAKA MASHABIKI WAJITOKEZA KUZISAPOTI AZAM NA SIMBA MICHUANO YA AFRIKA

Na Boniface Wambura

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) linawataka mashabiki wa mpira wa miguu kujitokeza kwa wingi wikiendi hii kuzishangilia timu za Azam na Simba zitakazocheza mechi za mashindano ya Afrika jijini Dar es Salaam.

Nguvu ya washabiki ni muhimu katika kuziweza timu hizo kufanya vizuri katika mechi hizo za nyumbani dhidi ya Al Nasir Juba ya Sudan Kusini na Club Libolo ya Angola.

Azam itacheza Jumamosi (Februari 16 mwaka huu) dhidi ya Al Nasir katika mechi ya Kombe la Shirikisho wakati Simba itaikabili Club Libolo kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayofanyika Jumapili.

Mechi zote zitachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


'BIG BOSS' KESHI ACHOMOA KUJIUZULU.



KOCHA wa timu ya taifa ya Nigeria, Steven Keshi ataendelea kuifundisha timu hiyo baada ya waziri wa michezo wa nchi hiyo Bolani Abdullahi kufanya mazungumzo ya kina na kocha huyo.

Mgogoro uliopo kati ya Keshi na Shirikisho la Soka la Nigeria-NFF lilipelekea kocha huyo mwenye umri wa miaka 51 kutangaza kujiuzulu katika kituo cha redio cha Metro FM nchini Afrika Kusini. Lakini mara baada ya waziri huyo kufanya naye mazungumzo jana jijini Johannesburg alifanikiwa kumshawishi kocha huyo kuendelea na kibarua chake ingawa haikufafanuliwa kwa undani mazungumzo yao yalihusiana na nini.

Pia kuna taarifa kuwa mazungumzo ya usuluhishi kati ya Keshi na NFF yataendelea wakati timu hiyo itakapowasili jijini Abuj leo.

VILLA AKIMBIZWA HOSPITALI.


MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Barcelona, David Villa amekimbizwa hospitali na kulazwa kutokana na matatizo ya figo na kuna uwezekano akakosekana katika mchezo wa La Liga dhidi ya Granada utalaochezwa Jumamosi ijayo. Katika taarifa iliyotumwa katika mtandao wa klabu hiyo mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Hispania anatarajiwa kufanyiwa upasuaji mdogo ili kutibu tatizo hilo la figo linalomsumbua. Villa alikuwa bado akipambana ili kurejea katika kiwango chake baada ya kuvunjika mguu katika michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia Desemba mwaka 2011.

Nyota huyo ameshafunga mabao matano katika michezo 15 ya ligi aliyocheza msimu huu na mabao matano mengine katika michuano ya Kombe la Mfalme lakini hajafunga bao lolote katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

No comments: