Monday, February 4, 2013

NIGERIA NA BUKINA FASO ZATINGA NUFU FAINALI AFCON


Kosi cha Nigeria
Kikosi cha Bukina Faso

 Timu ya Nigeria, Super Eagles, imetinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa kuilaza Ivory Coast 2-1.
Bao la kuongoza la Nigeria likiwekwa kimiani na Emmanuel Emenike dakika ya 42.

Ivory Coast ilisawazisha bao hilo baada ya mpira wa adhabu uliopigwa na Didier Drogba na kumfikia mfungaji Cheick Tiote katika dakika ya 51 na kuunganisjha kwa kichwa mpira huo.

Hata hivyo Nigeria ilipata bao lingine la pili katika dakika ya 78 likifungwa na Sunday Mba. Kosa la safu ya ulinzi ya Ivory Coast kumwaachia mfungaji kukokota mpira kwa muda mrefu ndiko kulikopeleka kilio kwa vijana wa Ivory Coast.

Kikosi cha Ivory Coast ambacho kilionekana kuwa ni bora zaidi katika michuano hii, kimeonekana kuendelea na mkosi wake kama ilivyokuwa mwaka jana wakitolewa katika fainali na Zambia, timu ambayo haikupewa nafasi.
Katika mpambano huo, Ivory Coast ndiyo iliyokuwa ikipewa nafasi zaidi kufuatia kikosi chake kusheheni majina makubwa kama vile Didier Drogba, Yaya Toure, Emmanuel Eboue, Gervihno, Kolo Toure, Cheick Tiote, Salomon Kalou na wengine wengi ndiyo yaliyowapa mashabiki wa timu ya Ivory Coast matumaini ya kusonga mbele.

Wachezaji wengi wa Ivory Coast kama vile Didier Drogba, Kolo Toure, Zokora na wengine wenye majina makubwa , huenda mashindano haya yalikuwa ya mwisho katika kuchezea timu yao ya taifa, kwani watakuwa na umri mkubwa na hivyo kutoshiriki michezo kama hii mwaka 2015.


Mchezo uliofuata ulikuwa ni kati ya Burkina Faso na Togo kukamilisha michezo ya robo fainali. 
Burkina Faso hatimaye imekuwa timu ya nne kufuzun kwa nusu fainali ya kuwania kombe la mataifa ya Afrika baada ya kuilaza Togo kwa bao moja kwa bila, katika mechi ya mwisho ya robo fainali.


Licha ya Togo kupigiwa upato kushinda, mechi hiyo sawa na ilivyokuwa katika robo fainali ya kwanza dhidi ya Ivory Coast na Nigeria, Burkina Faso ilifuzu kwa nusu fainali hizo.

Togo itajilaumu sana kwa kupoteza mechi hiyo, baada ya wachezaji wake kupoteza nafasi nyingi sana za kufunga wakati wa mechi hiyo.

Baada ya dakika tisini za kawaida kumalizika, hakuna timu iliyokuwa imeona lango la mwenzie hatua iliyopelekea mechi hiyo, kuongezwa muda zaidi.

Kunako dakika ya 105 Burkina Faso hatimae ikapata goli kupitia mchezaji wake Jonathan Pitroipa.

Pitroipa alifunga bao hilo kwa kichwa kufuatia mpira wa kona.

Burkina Faso sasa itacheza na Ghana katika nusu fainali ya pili siku ya Jumatano mwendo wa saa mbili na nusu majira ya Afrika Mashariki.

Nusu Fainali ya kwanza itakuwa kati ya Nigeria na Mali.

Kwa mwaka mwingine tena timu zilizosalia kwenye mashindano hayo, zinatoka Afrika Magharibi baada ya timu nyingine kutoka maeneo ya Kaskazini, Mashariki na Kusini kubanduliwa nje ya michuano hiyo.


No comments: