LIGI KUU TANZANIA BARA KUENDELEA KESHO NA KESHOKUTWA YANGA YASAKA KISASI CHA 3-0 KWA MTIBWA SUGAR KESHO SIMBA KUWAVAA JKT RUVU J'PILI
VINARA wa ligi kuu ya Vodacom, Yanga kesho watajaribu kulipa kisasi cha kipigo cha aibu cha 3-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar ya Morogoro wakati timu hizo mbili zitakaporudiana katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mechi yao ya awali iliyofanyika Septemba 19, 2012 kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, Yanga walikumbana na kipigo hicho kisichotarajiwa kilichosababisha uongozi wa klabu hiyo ya Jangwani umtimue kocha wao Mbelgiji Tom Saintfiet baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa siku 80 tu na kuiongoza kutwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame).
Mtibwa waliweka rekodi nzuri dhidi ya miamba ya soka nchini mzunguko wa kwanza baada ya kuwafunga pia Simba 2-0 kwenye uwanja huo huo na kumfanya kipa nahodha wa timu ya taifa, Juma Kaseja kumwaga kilio na wakati fulani alikaribia kuzipiga na aliyekuwa mshambuliaji wao Emmanuel Okwi katika tulio lililoonekana kupagawishwa na kichapo.
Mwamuzi Ronald Swai kutoka Arusha ndiye atakayechezesha mechi hiyo inayotarajiwa kuwa na upinzani mkali, kwani wakati Yanga ikiongoza ligi hiyo, wapinzani wao Mtibwa Sugar katika mechi iliyopita walilala mbele ya Polisi Morogoro ambayo ni ya mwisho katika msimamo wa ligi kwa sasa.
Polisi Morogoro itakuwa mwenyeji wa African Lyon kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro wakati Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Mgambo Shooting na Ruvu Shooting inayofundishwa na Charles Boniface Mkwasa.
Keshokutwa (Jumapili) kutakuwa na mechi mbili. Simba itaumana na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam huku Tanzania Prisons ikiikabili Coastal Union katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
NAYO LIGI DARAJA LA KWANZA KUANZA KUTIMUA VUMBI KESHO
Ligi Daraja la Kwanza (FDL) mzunguko wa pili inaanza kesho.
Villa Squad na Moro United zinaumana kesho (Februari 2 mwaka huu) Uwanja wa Karume, Dar es Salaam katika moja ya mechi za kundi B
Mechi nyingine ya Kundi B itakuwa Transit Camp na Ndanda itakayochezwa Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani.
Kundi A litakuwa na mechi kati ya Mbeya City na Burkina Faso itakayochezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Majimaji na Kurugenzi katika Uwanja wa Majimaji mjini Songea, na Polisi Iringa dhidi ya Mkamba Rangers kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa.
Kundi C ni Polisi Dodoma na Kanembwa JKT (Uwanja wa Jamhuri, Dodoma), Morani dhidi ya Mwadui (Uwanja wa Kiteto, Manyara), Polisi Mara na Pamba (Uwanja wa Karume, Musoma), Polisi Tabora na Rhino Rangers (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora).
Ligi hiyo inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa Machi mwaka huu ambapo mshindi wa kila kundi atapanda daraja kucheza Ligi Kuu msimu ujao.

No comments:
Post a Comment