WANANDOA MBARONI KWA KUDAIWA KUUA
![]() |
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi Dhahiri Kidavashari |
JESHI la Polisi wilayani Mpanda Mkoa wa Katavi, linawashikilia wanandoa wawili kwa tuhuma za kumuua Abdalla Kipeta (35), mkazi wa mtaa wa Kawajense, kwa kumchoma visu sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari, alisema tukio hilo, lilitokea juzi saa 1.30 usiku jirani na nyumbani kwa marehemu.
Aliwataja wanandoa hao, kuwa ni Patrick John (40) na mkewe Rehema Alexanda (32), wakazi wa mtaa wa Nsemlwa.
Alisema siku ya tukio, Abdalla alikuwa anatoka kwenye biashara yake ya duka akirejea nyumbani, ndipo aliposhambuliwa kwakuchomwa na visu na watuhumiwa.
Alisema watu hao, walichoma kwa kutumia kisu na kitu chenye ncha kali sehemu za kifuani, shingoni, mgongoni na tumboni na kusababisha utumbo wake kutoka nje.
Alisema majirani, walipokagua mwili wa marehemu walimkuta akiwa na fedha zake kwenye mfuko Sh 1,400,000. Ambapo simu yake ya kiganjani iliporwa na wauaji kama njia ya kuharibu ushahidi.
Alisema hivi karibuni, mtuhumiwa Patrick, alikuwa na ugomvi wa wivu wa kimapenzi na Abdalla kwa kumtuhumuwa kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mke wake Rehema.
Ugomvi wao, ulizidi kuongezeka siku hadi siku hali ambayo ilimfanya mtuhumiwa amtumie watu Abdalla akimtaka avunje uhusiano na Rehema.
Patrick pamoja na kumtumia watu wamkanye Abdalla, bado aliendelea na vitisho hali ambayo ilimfanya marehemu atoe taarifa kituo cha polisi cha Mpanda mjini.
Kamanda Kidavashari, alisema upelelezi utakapokamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani na ametoa wito wa watu kuacha tabia ya kujichukulia sheria mikononi.
Chanzo:Gazeti la Mtanzania
No comments:
Post a Comment