Friday, January 25, 2013


MZUNGUKO WA LALA KWA BURIANI  WA LIGI KUU TZ BARA KUANZA
WIKI ENDI HII

MZUNGUKO wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara unaanza kesho (Januari 26 mwaka huu) kwa raundi ya 14 ambapo timu 12 kati ya 14 za ligi hiyo zitakuwa katika viwanja sita tofauti.

Mabingwa watetezi Simba watakuwa wenyeji wa African Lyon katika mechi itakayochezwa saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Hiyo itakuwa mechi ya kwanza kwa Kocha wake mpya, Mfaransa Patrick Liewig anatarajiwa kwa mara ya kwanza kukiongoza kikosi hicho katika mechi ya VPL akisaidiwa na Moses Basena na Jamhuri Kihwelo.

Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro wenye uwezo wa kumeza watazamaji 8,000 ndiyo utakaohimili vishindo vya mechi kati ya Polisi Morogoro na wenyeji Mtibwa Sugar. Polisi Morogoro ambayo ni ya mwisho katika msimamo wa VPL ililazimisha suluhu katika mechi ya mzunguko wa kwanza.

Coastal Union itaoneshana kazi na wana-Tanga wenzao Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.

Timu zinazo katikati ya msimamo wa ligi, Ruvu Shooting na JKT Ruvu zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani.

Wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, Azam baada ya mechi za kirafiki nchini Kenya wanarejea kwenye Ligi Kuu ya Vodacom kwa kuikaribisha Kagera Sugar ya Kocha Abdallah Kibaden kwenye Uwanja wa Chamazi.

Ni mechi ya kulipa kisasi kwa Kagera Sugar baada ya kulala bao 1-0 katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa Septemba 15 mwaka jana Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba.

Maafande wa Oljoro JKT wanaanza kuchanga upya karata zao katika mzunguko wa pili kwa kuikaribisha Toto Africans ya Mwanza kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, jijini Arusha.

YANGA iliyopiga kambi ya mazoezi kwa takribani wiki mbili mjini Antalya, Uturuki itaanza mzunguko wa pili dhidi ya Tanzania Prisons katika mechi itakayochezwa keshokutwa (Januari 27 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Vinara hao wa VPL wakiongoza kwa tofauti ya pointi tano dhidi ya Azam wanaowafuatia wanaikabili Tanzania Prisons ambayo imetumia dirisha dogo kuongeza wachezaji wawili akiwemo mshambuliaji mkongwe Emmanuel Gabriel.

Timu hizo zilitoka suluhu katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, jijini Mbeya. Hivyo kiu ya washabiki ni kutaka kujua nani ataibuka mbabe kati ya timu hizo msimu huu.

No comments: