LALA SALAMA DARAJA LA KWANZA KUANZA JUMAMOSI
![]() |
Bonifasi Wambura |
Mzunguko wa pili wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ambayo itatoa timu tatu zitakazocheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao (2013/2014) unaanza Jumamosi (Februari 2 mwaka huu) katika viwanja tisa tofauti.
Kundi A litakuwa na mechi kati ya Mbeya City na Burkina Faso itakayochezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Majimaji na Kurugenzi katika Uwanja wa Majimaji mjini Songea, na Polisi Iringa dhidi ya Mkamba Rangers kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa.
Mechi za Kundi B, Jumamosi (Februari 2 mwaka huu) itakuwa Transit Camp na Ndanda itakayochezwa Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani, Moro United dhidi ya Villa Squad (Uwanja wa Karume, Dar es Salaam). Jumapili (Februari 3 mwaka huu) ni Tessema na Green Warriors (Mabatini, Pwani), Ashanti United na Polisi Dar (Uwanja wa Karume, Dar es Salaam).
Kundi C Jumamosi (Februari 2 mwaka huu) ni Polisi Dodoma na Kanembwa JKT (Uwanja wa Jamhuri, Dodoma), Morani dhidi ya Mwadui (Uwanja wa Kiteto, Manyara), Polisi Mara na Pamba (Uwanja wa Karume, Musoma), Polisi Tabora na Rhino Rangers (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora).
Ligi hiyo inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa Machi mwaka huu ambapo mshindi wa kila kundi atapanda daraja kucheza Ligi Kuu msimu ujao.
KABANGE TWITE KUSUBIRI MSIMU UJAO YANGA
Mchezaji Alain Kabange Twite hataweza kuichezea Yanga msimu huu (2012/2013) baada ya klabu hiyo kuingiza nyaraka zenye upungufu wakati ikimuombea Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa njia ya mtandao (Transfer Matching System- TMS).
Kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), baadhi ya nyaraka zenye upungufu katika maombi hayo ni mkataba kati ya Twite na Yanga, lakini vile vile makubaliano ya mkopo (Loan Agreement) kati ya Yanga na FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ambayo ndiyo inayommiliki mchezaji huyo.
Ili mchezaji aweze kupata ITC kwa njia ya TMS, kwa mujibu wa Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za TFF kuna nyaraka kadhaa muhimu zinatakiwa kukamilika katika maombi hayo ili hati hiyo iweze kupatikana.
No comments:
Post a Comment