KUSHAMBULIANA KWA WAKUU WA POLISI JIJINI DAR KUHUSU SWALA NA UKAHABA KUNATUPA PICHA GANI RAIA?
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, juzi makamanda wawili wa mikoa ya kipolisi ya Temeke na Kinondoni walikwaruzana hadharani.
Chanzo cha kukwaruzana kwao ni hatua ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Charles Kenyela kuendesha operesheni kuwakamata watu wanaofanya biashara ya ukahaba.Hata hivyo, mwenzake, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Engelbert Kiondo, alinukuliwa na vyombo vya habari juzi akimshambulia Kamanda Kenyela akidai kuwa amekurupuka kuendesha operesheni hiyo.
Kiondo alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kuwa haoni umuhimu wa Kamanda Kenyela kuwakamata makahaba hao, wakati hakuna sheria inayozuia biashara hiyo.
Pamoja na kudai kwamba hakumpinga, bali alijaribu kutoa maoni yake kuhusiana na kamatakamata hiyo, Kiondo alidai kwamba kuwakamata watu hao hakuwezi kukomesha biashara hiyo.
Kwa kweli Watanzania makini hawakutegemea jambo hili, hasa ikizingatiwa kwamba wao ni walinzi wakuu wa usalama katika maeneo yao, na watu walio chini ya kamanda mmoja wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Tunajiuliza, kulikuwa na sababu gani ya Kiondo kumshambulia mwenzake hadharani? Kama aliona kwamba Kamanda Kenyela amekosea, aliona ugumu gani kuwasiliana na mwenzake na kumpa ushauri huo? Ama aliona kero gani kufikisha ushauri huo kwa wakubwa wao ambao wangeweza kumwita Kenyela na kumpa mbinu mbadala?
Tujiulize tena, kuna nini katika suala hili la makahaba hadi watendaji hawa wakubwa katika medani ya usalama washambuliane na kudhalilishana?
Hakuna siri kwamba biashara ya ukahaba inazidi kushika kasi katika Jiji la Dar es Salaam, unaofanywa na watu wa rika na hali zote za vipato.
Hali katika barabara za jiji wakati za usiku ni ya kusikitisha kutokana na kuenea kwa misururu ya kina dada waliovaa nusu uchi.
Imefika mahali ambapo dada hao huvamia gari lolote linalosimama katika maeneo yao na kuanza kuongea matusi, huku wakifunua sehemu zao za siri kama njia ya kuvuta biashara zao, bila kujua wala kujali ndani ya gari kuna nani.
Makahaba hawa wanajua mahali pa kuwapeleka wateja wao, huko kwenye madanguro ambayo ndani kuna kila aina ya biashara.
Leo hii kuna wimbi kubwa la wizi na ujambazi. Kuna ongezeko kubwa la uuzaji wa mihadarati. Tunashuhudia wingi wa baa na grosari zinazoendesha biashara zake usiku kucha.
Kuna uwezekano mkubwa kwamba Kenyela amegundua ‘handaki’ wanakojificha wahalifu hawa. Na katika moja ya mbinu za mapambano ameanzia na kamatakamata hiyo ambayo kwa mikakati na mbinu zake itamsaidia kuufanya mkoa wake kuwa tulivu kwa kiasi fulani.
Tunataka wakubwa warekebishe hali hii ambayo inazidi kutia shaka utendaji kazi ndani ya Jeshi la Polisi na vitengo vyake.
Kauli hizi zinaweza kutafsiriwa kwa namna mbaya zaidi na Watanzania, hasa inapofika mahali jeshi hilo likakosa imani kwa wananchi.
Tunaungana na Kamanda Kenyela, ingawa tunamtaka aboreshe operesheni yake kwa kuangalia mambo makubwa na ya msingi yanayosababisha kuwapo kwa biashara hii.
No comments:
Post a Comment