Saturday, December 1, 2012

Nusu ya wanandoa hawaambukizani Ukimwi


 WANANDOA wanashauriwa kupima maambukizi ya Ukimwi ili kuongeza tahadhari kwa kuwa bado kuna uwezekano mkubwa wa mmoja aliyeathirika kutomwambukiza mwenzake.
Utafiti mpya juu ya maambukizi ya uganjwa huo umebaini kuwa, asilimia 47 ya watu walio katika mahusiano ya kimapenzi ambao mmoja anaishi na virusi vya Ukimwi, hawawaambukizi wenzi wao.
Kwa mujibu wa utafiti huo uliofanywa na madaktari bingwa wa nchini Uingereza na kuchapishwa katika Jarida la Magonjwa ya Kuambukiza la Lancet, si lazima kila mwenye ukimwi amwambukize mwenzake, ila kuchukua tahadhari ni muhimu.
Utafiti huo uliofanyika katika nchi 14 ikiwemo Tanzania, kwa kuchukua sampuli za wenza 13,061 katika nchi 27, ulibaini kuwa asilimia 47 ya wanawake na wanaume wenye Ukimwi walioko kwenye mahusiano ya kudumu, walikuwa na wenza ambao hawana VVU.
Jarida hilo limeeleza kuwa zipo sababu za kibaolojia na kisayansi zinazofanya baadhi ya watu wasiwaambukize wenzao Ukimwi.
“Hii ni pamoja na aina ya seli za mwanadamu, virusi na iwapo mmoja anatumia dawa za kufubaza makali ya Ukimwi au la,” linaeleza Jarida hilo.
Utafiti huo unafafana na uliofanywa na Benki ya Dunia (WB), chini ya Dk Damien de Walque katika nchi tano za Afrika, zikiwemo Kenya na Tanzania ambao ulibaini kuwa, robo tatu ya wenzi wanaoishi na VVU, mmoja hakuwa na maambukizi hayo.
Novemba mwaka huu, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema kuwa, karibu nusu ya watu wanaoishi na VVU walio katika mahusiano wana wenza ambao hawana maambukizi.
Akizungumza tafiti hizo, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana, Meshack Shimwale alisema zipo sababu nyingi zinazofanya mwenzi mmoja akawa na maaambukizi na wengine hana.
“Baadhi ya sababu hizo ni aina ya virusi, vichocheo, upekee wa maumbile, idadi ya wadudu na tabia zao,” alisemna kuendelea;
“Pia muda ambao mwenye virusi ameishi na virusi hivyo, iwapo anatumia ARV, au hatumii na majeraha katika sehemu za siri.”
Daktari huyo alibainisha kuwa kuna virusi ambavyo vipo hai na vina kasi kubwa ya kuingia katika mwili wa mtu kwa haraka na vingine si vikali. Virusi hivyo hufa kabla havijaingia katika majimaji ya mwili wa binadamu, alisema.
Na  Florence Majani  (email the author)

No comments: