Saturday, December 8, 2012

MWANAMUME(40) AMBAKA MTOTO (10)

Mwanafunzi wa Darasa la Tatu katika Shule ya Msingi Sombetini mwenye umri wa miaka 10 (jina limehifadhiwa) jijini Arusha, amelazwa katika hospital ya mkoa ya Mount Meru baada ya kubakwa na kuharibiwa vibaya sehemu zake za siri na mwanaume mwenye umri wa miaka 40, mtoto wa Diwani.
Akizungumza na vyombo vya habari, mama mdogo wa mtoto huyo, Fatuma Zuberi alisema kuwa tukio hilo ambalo limethibitishwa na Jeshi la Polisi jijini hapa, limetokea Novemba 30 mwaka huu majira ya saa moja jioni nyumbani kwao mtaa wa Pangani jijini hapa. Alisema kuwa siku ya tukio yeye na familia walienda kwenye sherehe za “kitchen party” na kumwacha mtoto huyo nyumbani akiwa na bibi yake.
Baada ya kutoka katika sherehe hiyo majira ya saa 4 usiku walimkuta mtoto huyo akiwa amelala chumbani bila nguo ya ndani na kumhoji. Mtoto huyo alisema hakuvaa chupi kwa kuwa ilikuwa inambana. Alieleza kuwa alimwamuru mtoto asilale bila kuvaa nguo ya ndani na kumtaka achukue nguo hiyo avae, lakini alipigwa na butwa baada ya kuona nguo hiyo ikiwa mbichi na imetapakaa manii na damu, ndipo aliposhituka na kutaka kumwadhibu mtoto huyo kutokana na mtoto huyo kutotaka kueleza kilichotokea. Hatimaye aliamua kumchapa na ndipo aliposema ukweli kwamba alibakwa na mwanaume aliyemtaja kwa jina la Thabit Jafari (40) ambaye imefahamikwa kuwa ni jirani yao na ni mtoto wa Diwani (CCM) wa Kata ya Mjini Kati bwana Abdulrasul Tojo. “Tulishangaa baada ya kuelezwa kuwa Jafari ndiye aliyehusika kumbaka mtoto wetu. Hatukuamini kwani kijana huyo ni jirani yetu na tumekuwa tukiishi naye kwa muda mrefu kama ndugu. Huyo ana familia yake na ana mtoto wa kike anayesoma kidato cha tatu.” alisema Fatuma. Alisema kuwa baada ya tukio hilo waliamua kumpigia simu kijana huyo na ndipo alipokiri na kueleza kuwa alifanya kitendo hicho baada ya kupitiwa na shetani na kuomba wamsamehe na kwamba hatorudia tena. Hata hivyo, hawakuridhika na maelezo ya kijana huyo kutokana na kuelezwa na mtoto huyo kwamba, tukio hilo halikuwa la kwanza kutokea kwani amekuwa akimfanyika tendo hilo mara kwa mara na mara nyingi humfanya majira ya usiku wakati mtoto anapoenda kuosha vyombo. Familia ya mtoto huyo iliamua kutoa taarifa Polisi baada ya kumweleza baba wa mtuhumiwa  Diwani wa Kata ya Mjini Kati na kushindwa kuwapa ushirikiano; Ndipo walipoamua kwenda katika Kituo cha Polisi cha Mjini Kati na kufungua jalada la kesi.

 --- Habari hii imeripotiwa na Joseph Ngilisho -Arusha via blogu ya Bertha

No comments: